JOPO
la madaktari 50 kutoka nchini India, wanatarajia kufanya maonesho ya
matibabu katika ukumbi wa Diamond Jubilee Agosti 30 hadi 31, mwaka huu,
kuanzia saa nne asubuhi hadi 11 jioni.
Taarifa
iliyotolewa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana na Balozi wa
India nchini, Bw. Debnath Shaw, ilisema maonesho hayo yameandaliwa na
Taasisi ya Shirikisho la Biashara nchini India la Medical Tourism
Destination (IMTD).
Aliwaomba
watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya wajitokeze katika maonesho
hayo ili waweze kupata huduma ya matibabu ambayo itatolewa katika ukumbi
huo kwa gharama za chini.
“Gharama
zao zitakuwa za chini na zitamwezesha kila mwananchi mwenye matatizo ya
kiafya kuzimudu na kupata huduma, India inaongoza duniani kwa kutoa
huduma bora za tiba.
“Nchi
yetu pia ina madaktari bingwa wanaoaminika katika utoaji huduma, mwaka
huu IMTD inawaleta watoa huduma kutoka hospitali kubwa za India ambazo
ni Fortis na Medanta,” alisema.
Alizitaja
hospitali nyingine kuwa ni Asian Heart, Seven Hills, SRM Hospital,
Vasan Eye Care na Idara ya Aayush ili kuja kuwasaidia wagonjwa waliopo
nchini.
Alisema
maonesho hayo pia yamelenga kutoa fursa ya wataalamu wa sekta hiyo
kufahamiana wakiwemo wasomi na wadau ili kuweka jukwaa kwa mashirika na
taasisi kati ya India na Tanzania waweze kushirikiana kuimarisha huduma
ya afya.
Alisema
watakuwepo wawakilishi kutoka hospitali na vituo vya afya vilivyopo
nchini humo kikiwemo kitengo cha upasuaji, hospitali za macho, ortho
care, bidhaa za afya, huduma za kiasili, utalii wa kiafya, kampuni za
dawa na vituo vya physiotherapy.
“Zaidi
ya nchi 30 duniani ikiwemo Marekani, Canada, Uingereza, Urusi,
Uarabuni, Uganda, Tanzania, Sri Lanka na nchi za Bara la Asia, huwa
wanakwenda India kupata matibabu,” alisema.
Bw. Shaw aliongeza kuwa, nchi hiyo pia inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watalii wanaokwenda kufuata matibabu.
Habari na Salim Nyomolelo