MUHTASARI WA TAARIFA YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YA UCHUNGUZI WA TUKIO LILILOPELEKEA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI KILICHOTOKEA SEPTEMBA 2, 2012 KIJIJINI NYOLOLO, WILAYA YA MUFINDI, MKOANI IRINGA
UTANGULIZI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni idara huru ya
serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 129(1)(c) cha Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya mwaka 2001. Jukumu kubwa la Tume
ni kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za binadamu nchini. Katika
kutekeleza jukumu hilo Tume imepewa mamlaka ya kupokea malalamiko (kwa
njia mbalimbali) kutoka kwa mtu yeyote au kuanzisha uchunguzi wake
yenyewe endapo itaona kuna uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa
misingi ya utawala bora.
Kwa kuzingatia majukumu hayo, Tume ilianzisha uchunguzi wake yenyewe
baada ya vyombo vya habari kutoa taarifa ya tukio la kifo cha Daudi
Mwangosi. Tume iliunda timu ya watu watatu iliyoongozwa na Mhe. Kamishna
Bernadeta Gambishi akisaidiwa na maafisa wawili, Bwana Gabriel
Lubyagila na Bwana Yohana Mcharo. Timu hiyo ilifanya uchunguzi wake
kuanzia tarehe 13-19 Septemba, 2012.
Katika uchunguzi uliofanywa, Tume ilizingatia zaidi masuala ya uvunjwaji
wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Hivyo
basi, Tume ilitilia maanani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
sheria mbalimbali za nchi na mikataba ya kimataifa na ya kikanda
inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.
Kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya Tume Na. 7 ya mwaka 2001, baada ya
uchunguzi huo kukamilika, Tume imeandaa taarifa yake na kuiwasilisha
kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Taarifa ya uchunguzi wa Tume imegawanyika katika sehemu kuu nne, ambazo
ni:
Maelezo ya viongozi, watendaji na wananchi waliohojiwa
Uchambuzi wa taarifa/vielelezo vilivyopokelewa kwa kuzingatia
sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki
za binadamu
Matokeo ya uchunguzi
Maoni na mapendekezo.
Kwa kuwa tukio la kifo cha Daudi Mwangosi liligusa hisia za jamii, Tume
imeona ni vyema kukutana na wawakilishi wa vyombo vya habari ili kutoa
taarifa yake.
2.0 MATOKEO YA UCHUNGUZI
Katika uchunguzi wake Tume imebaini kuwa:
Tarehe 02/09/2012 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kiliruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi (OCD) kufanya
mikutano ya ndani na kuzindua matawi mapya. Lakini jioni ya tarehe
01/09/2012 Kamanda wa Polisiwa Mkoa wa Iringa (RPC), alizuia CHADEMA
kufanya mikutano iliyoruhusiwa na OCD ambaye ni “Officer In-charge” wa
polisi wa eneo husika kama sheria inavyotaka.
Viongozi wa CHADEMA walikuwa na mazungumzo na Mkuu wa Polisi
Mkoa Upelelezi (RCO) na kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa na
mikutano ya hadhara.
Msajili wa vyama vya siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama
vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa.
Wakati shughuli za uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, RPC
alifika katika eneo hilo na kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe; na
kuwa wafuasi wa CHADEMA walipingakukamatwa kwa viongozi wao.
RPC aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya
wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.
Baada ya mabomu ya machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na
kukimbia ovyo; na kuwa marehemu Daudi Mwangosi alizingirwa na askari,
aliteswa na hatimaye inadaiwaalipigwa bomu na kufa hapo hapo.
Daudi Mwangosi aliuwawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo
Ofisi ya CHADEMA tawi la Nyololo.
Katika tukio hilo wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu,
wakiwemo Mwandishi wa Habari wa Nipashe, Bwana Godfrey Mushi, Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya Mufindi, Bibi Winnie Sanga na
Mkuu wa Kituo cha PolisiMufindi, Asseli Mwampamba aliyekuwa akifanya
jitihada zakumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.
Kutokana na hayo yote, Tume imejiridhisha kuwa tukio lililopelekea kifo
cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
2.1 Uvunjwaji wa Haki za Binadamu
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu
(Universal Declaration of Human Rights of 1948), Mkataba wa Kimataifa
kuhusu haki za kiraia na kisiasa (International Covenant on Civil and
Political Rights of 1966) na Mkataba wa mataifa ya Afrika kuhusu Haki za
Binadamu na Watu (African Charter on Human and Peoples Rights of 1981),
Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki zifuatazo:
Haki ya kuishi,
Haki ya kutoteswa na kupigwa,
Haki ya usawa mbele ya sheria na
Haki ya kukusanyika na kutoa maoni.
CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina usajili wa kudumu. Chini ya
sheria ya vyama vya siasa (Cap. 258 RE. 2002), vyama vya siasa vyenye
usajili vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya
kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa “Afisa wa Polisi” wa eneo husika.
Baada ya taarifa kutolewa chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi na
“security agencies” (mawakala wa usalama).
2.2 Ukiukwaji wa Misingi ya Utawala Bora
Ili pawepo utawala bora mamlaka zote za serikali ni lazima zifuate
utawala wa sheria. Uchunguzi umebaini kuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Michael Kamuhanda tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji wa
majukumu yake alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002)
kifungu cha 11(a) na (b) na sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia
kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA
wakati yeye hakuwa “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika. Kwa
maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu
ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi
mabaya ya mamlaka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Aidha, hatua ya Msajili wa vyama vya siasa, Mhe. John Tendwa kuwaandikia
barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa
sababu ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo
yaliyotolewa ndani ya barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Na. 1
ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati
wa sensa pia ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002)
Kifungu cha 11(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya
shughuli zake bila ya kuingiliwa.
Ibara ya 8(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelezea
kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na Haki ya
Kijamii, aidha ibara 18(b) na (c) ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo
haki ya kufanya mawasiliano (kutoa maoni/habari) na haki ya
kutoingiliwa katika mawasiliano yake. Haki hii imekiukwa kwa kiasi
kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Nyololo Mufindi kwa kuwa
waandishi wa habari na wafuasi wa CHADEMA walizuiwa na Polisi kufanya
shughuli zao za kupata habari na za kisiasa. Huu ni ukiukwaji wa
misingi ya utawala bora kwa kuwa hali hiyo inazorotesha au inafifisha
uhuru wa habari.
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO
Kwa kuzingatia Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7
ya mwaka 2001 Kifungu cha 15(2)(c) na 28 Tume inapendekeza yafuatayo:
Kamati za ulinzi na usalama za Mkoa na Wilaya ziwe makini na
vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wamisingi ya
utalawa bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao.
Aidha, kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali
zao kwa kujadili masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa
na vyombo vinavyotekeleza sheria.
Viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao waepuke malumbano na vyombo
vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa navyombo hivyo bila shuruti.
Pale wanapogundua kuwa pana uonevu au upendeleo ni vyema busara
ikatumika ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya
maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi auupendeleo miongoni mwa
jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria. Mfano, Jeshi la
Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo
huoChama cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakifanya uzinduzi wa Kampeni huko
Zanzibar. Aidha, rai ya Msajili wa vyama vya siasa haikuzingatiwa kwa
upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA walishurutishwa na Polisi kutii rai
hiyo.
Demokrasia ya mfumo vya vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.
Elimu ya vyama vya siasa na sheria ya Polisi kuhusu vyama vya
siasa itolewe kwa askari polisi ambao wanaonekana kutozifahamu kabisa.
4.0 HITIMISHO
Jukumu la kulinda amani na utulivu ni wajibu wa kila mtanzania, mkulima
na mfanyakazi, viongozi wa serikali na watumishi wa umma wote wanapaswa
kuwa wazalendo wa kweli wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Tume inatoa wito kwa watanzania wote kuheshimu haki za binadamu na
kutekeleza kwa vitendo misingi ya utalawa bora. Kwa kufanya hivi Taifa
letu litaendelea kuwa na amani na utulivu. Tume inatoa rai kwa jeshi la
polisi kutekeleza wajibu wake mkuu wa ulinzi na usalama wa raia bila
kutumia jazba.
Kuwepo kwa vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukuwa kwa demokrasia na sio
kuwa ni upinzani kwa chama tawala.
....................................................
Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri R. Manento
MWENYEKITI
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
OKTOBA 10, 2012