Jana majira ya saa mbili usiku, msanii na mchekeshaji maarufu nchini Sharo Milionea amefariki dunia kwa ajali mbaya ya gari wakati akitoa Dar es Salaam kueleka wilayani Muheza, Tanga.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Costantine Massawe Hussein Ramadhani au Sharo Milionea alikuwa akiendesha gari namba T478 BVR Toyota Harrier. Alipofika maeneo ya maguzoni njekidogo na wilayani MUHEZA gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa, likagonga mti na kusababisha kifo chake na yeye kutokea mbele ya kioo cha gari na kutupwa mbali.
Alisema Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali Teule ya wilaya ya Muheza. Aliongeza kuwa hakuna kona kali wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali. Gari lake imehifadhiwa mahali salama kwakuwa limeharibika vibaya na kwamba kwenye gari alikuwa mwenyewe.
Habari kuhusu kifo chake zilianza kuenea jana usiku ambapo kwa upande wa rafiki yake wa karibu Kitale amesema alikuwa akiipiga simu ya Sharo Milionea iliyokuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa na kisha kupigiwa simu na Tundaman, Mzee Majuto na Mjomba wake Sharo kumtaarifu juu ya kifo hicho.
“Sisi binadamu tunaweza kuwaza hivi na Mungu naye akawaza lake kwahiyo sisi tunaziombea familia hizi Mungu azipe faraja ya kweli na faraja ya kweli nadhani inatoka kwa Mungu,”rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania , TAFF Simoni Mwakifwamba ameiambia TBC.
Kwa upande wake Steve Nyerere amesema kifo cha Sharo Milionea kimetokea wakati ambao alikuwa ameanza kufanikiwa. “Sharo umri wake na mambo aliyoanza kuyafanya ni makubwa. “Sharo alishaanza kupata matumaini yaani ni sawasawa unatupa mbegu halafu uitegemee inaanza kuchepua. Sharo alishaanza kuchepua, anachepua ile mbegu yake, ameanza kujisaidia yeye kama yeye sababu katika maisha lazima kwanza uanze kujisaidia wewe kama wewe halafu pili uingalie jamii inahitaji nini kwako. Amejipatia usafiri maskini ya Mungu, pa kulala, na maisha yote ya kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga kuwaona wazazi kutumia gharama yake.”
Steve amesema jambo la msingi ni kumwachia Mungu na kuondoa mawazo mabaya kuhusiana na kifo chake.
Umoja wasanii wa filamu nchini umesema umepata pigo kubwa hasa kwakuwa bado wana msiba wa msanii mwingine wa filamu, John Stephano ambaye anatarajia kuzikwa leo. Umesema baada ya mazishi hayo kesho watasafiri kwa mabasi mawili kuelekea wilayani Muheza kwaajili ya mazishi.