Waziri Mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras
Kwa kuzingitia kipimo kinachoanisha sifuri - kama kiwango kibaya zaidi cha rushwa - mpaka 100 - ikiwa ndiyo rikodi nzuri kabisa, Dernmark, Finland na New Zealand zimefungana kwa kupata alama 90. Lakini Afghanstan, Korea Kaskazini na Somalia kila moja imepata alama 8.
Hali ilivyo katika mataifa ya Kiarabu
Pamoja na hayo, ripoti hiyo imeonesha kumekuwa na mafanikio kidogo sana katika mataifa ya Kiarabu yaliyokumbwa na vuguvugu la kisiasa. Mataifa hayo ni pamoja na Misri na maeneo mengine ya Mashariki ya Kati.
Mataifa ambayo ni kiini cha mgogoro wa madeni yameendelea kupata alama duni zaidi, ambapo tatizo hilo la mgogoro wa madeni limeonekana kama chachu ya vitendo vya rushwa. Ugiriki imepata alama 36, Italia 42, Ureno 63 na Uhispania 65.
Mkurugenzi Mkuu wa Transparency International, Cobus de Swardt, ameyataka mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani yanapaswa kuonesha mfano kwa kuhakikisha taasisi zake zinasimamia uwazi na kwamba viongozi wanawajibika katika hilo.
Mataifa ya Magharibi yanayoongoza kiviwanda, kama Uswis, Canada, Australia na Sweden yanashikilia tena ile nafasi yake ya kuwa safi katika kudhibiti tatizo la rushwa. Lakini China, kama taifa namba mbili kwa nguvu za kiuchumi duniani limepata alama 39.
Taifa kubwa kabisa lenye nguvu za kiuchumi duniani Marekani limepata alama 73 na Ujerumani, ambalo ni taifa lenye uchumi mkubwa kuliko yote barani Ulaya, ikiwa na alama 79. Urusi, pamoja na kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili yake, inaonekana kufanya jitihada kidogo sana katika kukabiliana na tatizo la rushwa. Taifa hilo limeshika nafasi ya 133 katika nchi 176 katika kudhibiti rushwa kwa mujibu wa utafiti wa mwaka huu wa Transparency International.