Macho na masikio ya Watanzania leo yataelekezwa kwa Waziri wa
Fedha, Dk William Mgimwa wakati atakapoisoma hotuba ya Bajeti Kuu ya
Serikali kuanzia saa 10.00 jioni bungeni, mjini Dodoma.
Sambamba na Mgimwa, pia mawaziri wa fedha za nchi za Kenya na Uganda nao katika muda huo watasoma bajeti za nchi zao.
Waziri mpya wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich
atasoma bajeti ya kwanza ya nchi hiyo ikiwa chini ya utawala mpya wa
Rais Uhuru Kenyatta wakati ya Uganda itasomwa na Waziri wa Fedha, Maria
Kiwanuka.
Mwelekeo wa Bajeti
Dk Mgimwa aliwaambia waandishi wa habari, Dodoma
jana kuwa Serikali imetenga kiasi cha Sh18.2 trilioni kwa ajili ya mwaka
ujao wa fedha wa 2013/14.
Alisema wameweka vipaumbele kadhaa ambavyo ni nishati vijijini, miundombinu, maji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Bajeti hiyo itatanguliwa na ile ya mwelekeo wa
hali ya uchumi ambayo itasomwa asubuhi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Dk Mgimwa alisema wananchi hasa wa vijijini watapata huduma ya maji hasa baada ya kuongezwa Bajeti ya Wizara ya Maji.
Awali, wabunge waligomea Bajeti ya Maji ya Sh398
bilioni kabla ya kuongezwa hadi kufikia Sh582.5 bilioni ikiwa ni
ongezeko la Sh184 bilioni.
Waziri Mgimwa alisema pia kuwa suala la nishati ya
umeme ni kipaumbele kingine cha Serikali na kwamba itaisambaza katika
maeneo mbalimbali nchini na zaidi katika maeneo ya vijijini chini ya
Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Alisema kipaumbele kingine ni usambazaji wa
pembejeo za kilimo vijijini ili kuwasaidia wakulima kulima mazao bora.
Pia alisema katika mwaka huu wa fedha Benki ya Wakulima itaanzishwa ili
kutoa mikopo yenye unafuu ya kilimo.
Aidha, Serikali ilikwishatangaza vipaumbele
vingine ambavyo ni ujenzi wa Bandari za Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na
Bagamoyo, reli, elimu, Mfumo wa Teknolojia ya Mawasiliano (ICT), afya na
ujasiriamali.