Dar es Salaam. Saratani imeendelea kuwa tishio hapa nchini huku
hofu ikiendelea kuikumba jamii kutokana na wataalamu wa afya kushindwa
kufahamu tiba halisi ya maradhi hayo hatari.
Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road
zinaonyesha ongezeko la saratani ya mdomo na koo kwa kiasi kikubwa
kutoka kesi 167 mwaka 2006 hadi 277 mwaka 2012.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Ocean road, Julius
Mwaiselage anaeleza kuwa watanzania wasipende kuiga mambo ambayo si
sahihi bila kujua madhara yake kama kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo.
“Saratani ya mdomo ipo, na nyingine zinasababishwa na zinaa “ anasema Dk
Mwaiselage
Tafiti mbalimbali zimewahi kufanyika nchini na
kubaini kuwepo kwa ongezeko la saratani ya mdomo.Utafiti uliofanywa na
Dk Innocent Mosha wa Kitengo cha Patholojia cha Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH), umebaini aina za saratani 1,594, kati ya hizo 509
zikiwa ni za midomo kwa mwaka 2003 pekee.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kati ya saratani 509
za mdomo, saratani 242 zilisababishwa na Virusi vya Human Papiloma
ambavyo hutokana na zinaa.
“Ninachojua mimi ni kuwa Virusi vya HPV
husababishwa na magonjwa ya zinaa, hivyo mtu anayeugua saratani ya aina
hiyo, imetokana na zinaa,” anasema Dk Mosha.
Takwimu hizo ni zile zilizopatikana kwa watu waliokwenda kufanyiwa uchunguzi katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Dk Mosha anasema kuwa wanaume ndiyo huathiriwa
zaidi na saratani ya mdomo ambapo kwa hapa nchini, asilimia 53 ya
wanaume waliofika MNH kwa ajili ya vipimo, walibainika kuugua saratani
hiyo, huku wanawake wakiwa ni asilimia 47.
Utafiti kama huo ulifanywa pia na Dk Amos
Mwakigonja, mkuu wa Idara ya Patholojia katika Chuo Kikuu cha Tiba cha
Muhimbili (MUHAS).
Dk Mwakigonja alifanya utafiti wa saratani ya
mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma ambapo wagonjwa 78 walibainika na
saratani hiyo kuanzia mwaka 1990 hadi 2003. “Saratani za mdomo zipo za
aina nyingi na zimetofautiana kulingana na visababishi vyake,” anasema
Dk Mwakigonja.
Katika utafiti wake Dk Mwakigonja alibaini kuwa
wanawake wengi walikuwa na saratani ya mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma
kuliko wanaume.
Hata hivyo, utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia
50 ya wanaume walikuwa na saratani ya mdomo hatari zaidi (systemic)
kuliko wanawake ambao ni asilimia 37.