Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ametuma
ujumbe kwa wale wanaoitishia Tanzania. Amewaambia wakithubutu watakiona
cha mtemakuni kama ilivyokuwa kwa Idd Amin wa Uganda.
Alisema mamlaka za ulinzi na usalama zilimdhibiti
Amin alipofanya uvamizi katika ardhi ya Tanzania mwaka 1978 na kwamba
hazitashindwa kufanya hivyo kwa mtu mwingine yeyote atakayechezea
usalama wa nchi.
Wakati Rais akisema hayo, Mkuu wa Majeshi,
Jenerali Davis Mwamunyange amewahakikishia wananchi kuwa wakati wote
jeshi liko imara na kuwataka wasiogope lolote.
Viongozi hao walisema hayo jana katika maadhimisho
ya Siku ya Mashujaa iliyofanyika katika Kambi ya Jeshi ya Kaboya
iliyopo Muleba, Kagera.
“Sihitaji kusema tena, mmeshamsikia Mkuu wa
Majeshi, atakayejaribu atakiona cha mtemakuni, laleni usingizi na msiwe
na wasiwasi, msisikilize maneno ya mitaani,” alisema Rais Kikwete na
kuongeza:
“Wakati wowote, saa yoyote tuko tayari kulinda
nchi yetu. Hatuko tayari kuona amani inaharibika nchini, hatuwezi
kuruhusu mtu yeyote kuimega au kuichezea nchi yetu kama alivyofanya Idd
Amin.”
Katika siku za karibuni kumekuwa na kauli kadhaa
kutoka kwa baadhi ya viongozi wa nchi jirani ambazo zinatafsiriwa na
wananchi kwamba ni za kuitisha Tanzania.
Jenerali Mwamunyange alisema jeshi wakati wote
liko imara kuwalinda wananchi na nchi kwa jumla hivyo
wasiogope...“Endeleeni na shughuli zenu na msiogope mtu yeyote, fanyeni
kazi zenu bila wasiwasi.”
Huku akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria
maadhimisho hayo, Jenerali Mwamnyanye alisema yeyote atakayethubutu
kuchezea usalama wa nchi atakiona cha mtema kuni.
Akizungumzia Siku ya Mashujaa, Rais Kikwete
alisema ni siku ya kuwakumbuka mashujaa waliojitolea maisha yao wakati
wa Vita ya Kagera kuilinda nchi yao ili iwe salama na yenye amani.
“Kuhakikisha usalama wa nchi kuna gharama yake
kwani kuna wengine walikufa na wengine wakabaki na vilema kwa ajili ya
hilo. Wale ambao wamebaki na wana matatizo lazima tuwaangalie vizuri na
vile ambavyo havijafanyika tutavishughulikia kwani kutetea taifa ni kazi
ngumu.”
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi
mbalimbali wakiwamo, Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar,
Dk Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande na Jaji Mkuu wa
Zanzibar, Omar Othman Makungu ambao wote walipewa nafasi ya kuwasalimia
wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo.