Mazoezi yamekolea, uwanja wa Ushirika Moshi. |
Uhuru Suleiman amesifiwa na kocha kuwa ni kiungo mwenye kasi nyingi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. |
Mshambuliaji anayetumia mguu wa kushoto kutoka
Uganda, Yayo Lutimba Kato amefunga bao lake la kwanza tangu kujiunga na Coastal
Union ambayo imeweka kambi mjini Moshi tangu jana.
Kato ambaye ametoka URA inayoshiriki ligi kuu nchini
Uganda, alipatia timu yake bao la kuongoza dhidi ya Machava FC kwenye uwanja
wa Ushirika mjini humo, bao hilo alilifunga kwa ufundi mkubwa katika kipindi
cha pili baada ya kupokea pasi murua na kupiga shuti kali akiwa nje ya 18.
Akitoa taarifa kutoka Moshi, mwenyekiti wa Wagosi
Hemed Hilal ‘Aurora’ amesema “Katika dakika za lala salama mchezaji Atupele
Green, ambaye ameonyesha kiwango cha hali ya juu katika kipindi cha hivi
karibuni aliipatia Coastal Union bao la pili kabla ya Danny Lyanga kumalizia la tatu na kukifanya kikosi cha Wagosi wa
Kaya kuondokana na uhaba wa mabao ambapo tangu mechi ya kwanza ya kirafiki
mpaka sasa haijawahi kupata ushindi wa bao zaidi ya moja.”
Kabla mpira kuisha mwamuzi wa mechi ya leo aliwapatia
penati Wagosi baada ya mchezaji wao kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari,
lakini Yayo Kato alikosa penati hiyo na kuwanyima wenzake ushindi mnono wa 4-0.
Itakumbukwa mechi ya kwanza ya kirafiki walicheza na
URA ya Uganda wakatoka na ushindi wa bao 1-0, mechi ya pili walishuka dimbani
dhidi ya wekundu wa msimbazi Simba na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, wakati
mechi ya tatu walitoka suluhu ya 1-1 dhidi ya 3 Pillars ya Nigeria.
Aidha mechi ya nne ya kirafiki waliyocheza mjini
Mombasa Kenya, walimaliza kwa suluhu ya 1-1, wakati mechi ya leo ni ya tano ya
kirafiki kabla ya kuanza msimu wa ligi kuu ya soka Vodacom keshokutwa Agosti 24
jumamosi, ambapo Wagosi watafungua ligi mjii Arusha dhidi ya JKT Oljoro katika
uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.
Tukiweka kumbukumbu sawa tangu Coastal Union irudi
kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara huu utakuwa ni msimu wa tatu ambapo msimu
wa kwanza ilimaliza ikiwa imeshika nafasi ya tano, msimu wa pili ikashika
nafasi ya sita wakati msimu huu wamedhamiria kufanya makubwa kutokana na aina
ya kikosi walichonacho.
COASTAL UNION
AGOSTI 22, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA