Korogwe
WANANCHI wa Kijiji cha Mswaha Darajani Kata ya Mswaha wilayani Korogwe mkoani Tanga wamekataa kuupokea mradi wa umwagiliaji wa kijiji hicho kwa madai ya kujengwa chini ya kiwango.
Hatua ya wananchi hao waliiweka bayana katika mkutano wa kijiji hicho ambao ulifanyika Novemba 7 mwaka huu katika mradi huo uligharimu zaidi ya milioni 42 kuanzia hatua za awali mpaka mwisho.
Kilichopelekea mradi huo kukataliwa na wananchi hao mbele ya diwani wa Kata hiyo,Aweso Omari ambaye aliambatana na Afisa Mtendaji wa Kata hiyo Paulo Mzava kilitokana na ukuta wa kukingia maji uliojengwa kumepasuka na hivyo kushindwa kutumika licha ya kugharimu fedha hizo.
Akizungumza katika mkutano hao mmoja ya wananchi hao ,Juma Mussa alisema wanamuomba mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwapelekea wataalamu ili waangalie jinsi mradi huo ulivyohujumiwa ikiwemo kuchukuliwa hatua wahusika.
“Ninaamini endapo Mkurugenzi wa Halamshauri atakuja kuangalia mradi huo yatapatikana mafanikio ikiwemo kulipatia ufumbuzi suala la mradi huo “Alisema Mussa.
Mussa alifika mbali zaidi kwa kumuomba mkuu wa wilaya ya Korogwe,Mrisho Gambo kutembelea eneo hilo ili ajionee jinsi mradi huo ulivyoharibika na kushindwa kufanya kazi huku wananchi wakiendelea kuteseka.
Akizungumzia mradi huo,Diwani Aweso alisema mradi huo ulitengewa sh.milioni 35kwa ajili ya utengenezaji huo wa mradi ambao ulipagwa kutumika kwenye shughuli za umwagiliaji kwenye mbuga ya mswaha darajani.
“Baada ya kuchelewa kwa mradi huo nililazimika kumtafuta diwani wa kata hiyo Aweso ambapo alinijibu kuwa mradi huo utapasuka muda wowote ule kutokana na kujengwa chini ya kiwango“Alisema Aweso wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili.
Aweso alisema mkandarasi aliyepewa kujenga mradi huo alijenga chini ya kiwango hali ambayo ilipelekea kushindwa kufanya kazi ipasavyo badala yake kupasuka na kuendelea kuwapa tabu wananchi wa maeneo hayo.