Jambo jingine jipya ni kupunguzwa kwa madaraka ya uteuzi ya Rais kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam.Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa Rasimu ya Pili ya Katiba ikiwa na mambo sita mpya, huku ikiendelea kupendekeza Muungano wa Serikali tatu na kurejea kwa nchi ya Tanganyika.
Rasimu hiyo ya Pili ambayo imetolewa miezi saba baada ya Rasimu ya Kwanza, ilikabidhiwa jana kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Akizungumza kabla ya kukabidhi rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema ina Ibara 271, tofauti na ile ya kwanza iliyokuwa na Ibara 240.
Alisema ripoti ya rasimu hiyo pia ina maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, sera, sheria na utekelezaji maoni ya Mabaraza ya Katiba, takwimu za ukusanyaji wa maoni ya wananchi, makala za utafiti kuhusu mabadiliko ya Katiba na viambatanisho vya ripoti ya mabadiliko ya Katiba.
Mambo mapya
Maeneo yaliyofanyiwa marekebisho baada ya mchakato wa Mabaraza ya Katiba yaliyokutana kuanzia Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu ni kuongezwa kwa vipengele kuhusu haki za binadamu.
Miongoni mwao ni haki ya kutoa na kupata habari. Pia imetaja haki za makundi maalumu yakiwamo ya watoto, vijana, wazee, walemavu na wanawake.
Kuhusu uraia, Jaji Warioba alisema imependekezwa uraia wa Tanzania kuwa mmoja tu na kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na wa kujiandikisha wa nchi moja. Alisema imependekeza pia kutoa fursa kwa uraia wa nchi mbili.
Jambo jingine jipya ni kupunguzwa kwa madaraka ya uteuzi ya Rais kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.
Aidha, alisema rasimu hiyo imependekeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iwe taasisi inayojitegemea badala ya kuwa sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kama ilivyokuwa katika Rasimu ya Kwanza.
“Rasimu inapendekeza kuwepo na Jeshi moja la polisi na Idara moja ya Usalama kwa taifa zima, siyo kama tulivyokuwa imependekezwa katika rasimu ya kwanza kwamba kila upande unaweza kuanzisha jeshi lake la polisi,” alisema.
Muungano
Akizungumzia Muungano na jinsi Tume ilivyofanya uchambuzi wa pendekezo lake la Serikali tatu alisema: “Katika Rasimu ya Kwanza tulieleza kuwa kuendelea kwa Serikali mbili kulihitaji ukarabati mkubwa ambao tuliona hautawezekana.