Takriban watu elfu moja wameuawa na waasi wa zamani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mapambano yaliyodumu kwa siku mbili yaliyojitokeza mwezi huu, makadirio haya yanazidi yale ya Umoja wa Mataifa. Shirika la Amnesty International limesema.
Shirika hilo limesema kuwa uhalifu wa kivita bado unaendelea kufanyika nchini humo.
Wapiganaji hao ambao wengi wao ni Waislamu walimuondoa madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, Francois Bozize mwezi March, hali iliyosababisha mgogoro ndani ya jamii nchini humo.
Kiongozi wa waasi Michel Djotodia hivi sasa ni kiongozi wa kwanza kutoka jamii ya Waislamu anayeongoza taifa lenye Wakristo wengi na ndiye kiongozi wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya kati.
Katika ripoti hiyo, Amnesty International imesema waasi wa zamani wa Seleka waliwaua takriban watu 1000 mjini Bangui, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kulipa kisasi dhidi ya wapiganaji wa Kikristo wanaodaiwa kuwashambulia waasi wa Kiislam.
Idadi ya waliopoteza maisha imeelezwa kuongezeka kuliko ile iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ambao ulisema watu 450 waliuawa mjini Bangui na wengine 150 sehemu nyingine nchini humo.
Mashambulio hayo yamekuja baada ya wanamgambo wajulikanao kwa jina la anti-balaka ambao walikuwa wakiingia kila nyumba na kuwaua watu 60 wa jamii ya Kiislamu. Amnesty International imeeleza.
Mashambulio yaliyofanywa na wanamgambo wa zamani wa Seleka yamehusisha mauaji pia uvamizi na uporaji katika nyumba za raia,ambapo wanawake na watoto kadhaa wameuawa.
Shirika hilo limesema kuwa raia huuawa kila siku mjini Bangui, ingawa kumekuwepo na vikosi vya Ufaransa na Umoja wa Afrika, Ufaransa ikiwa na askari 1,600 nchini humo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema wapiganaji wa Kikristo walishambulia jamii ya kiislamu kaskazini mwa mji wa Bossangoa na kuwachinja watoto huku wakiwashinikiza wazazi wao kushuhudia mauaji hayo.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Djotodia aliiambia redio ya Kifaransa kuwa yuko tayari kuzungumza na viongozi wa wanamgambo wa Kikristo ili kutatua mzozo huo.
Kauli hiyo imekuja baada ya Umoja wa Afrika kuidhinisha kuongeza vikosi vyake na kufikia askari 6,000.
Vikosi vya Umoja wa Afrika na vya Ufaransa vinafanya jitihada za kuwanyang'anya silaha wanamgambo hao.