Dar es Salaam. Tasnia ya sanaa imeendelea kuandamwa na changamoto nyingi ikiwamo wasanii kununua stika za kazi zao kwa pauni ya Uingereza badala ya shilingi ya Tanzania.
Mfumo huo wa ununuaji wa stika zinazobandikwa katika makasha ya kazi zinazoandaliwa na wasanii hao hutolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ambayo imethibitisha jambo hilo, huku ikieleza kuwa wanauza kwa pauni kwa sababu mtengenezaji wa stika hizo akaunti yake ipo mwenye pauni, siyo shilingi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasambazaji wa kazi hizo, wasanii na uongozi wa sanaa nchini walisema tangu kuanza rasmi kwa mfumo huoJulai 2013, kumekuwa na hali ya sintofahamu kutokana na stika hizo kuwa adimu na zinapopatikana kuuziwa kwa fedha za nje kinyume na makubaliano ya serikali na wasanii juu ya mfumo huo.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff), Simon Mwakifamba alisema stika hizo kuuzwa kwa pauni ni changamoto mpya inayoukumba mfumo wa urasimishaji wa kazi za wasanii na kupoteza maana nzima ya zoezi hilo.
“Limekuwa ni tatizo kubwa linalowakwaza wasanii nchini hasa wasambazaji wa kazi hizo kutokana na gharama kubwa wanayotumia sambamba na kukosa stika kwa wakati mwafaka,” alisema na kuongeza;
“Mtu umeshajipanga kutoa kazi ziku mbili kabla, ukienda TRA unaambiwa stika zimekwisha wakati tayari umeshachukua mkopo benki yaani unakuwa umeongeza matatizo mengine juu.”
Mwakifamba alitoa wito kwa serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha inarekebisha mfumo huo uliopo sasa ambao umeonekana kuwa kero kwa wasanii.
“Naona kutumia pauni ni kuongeza gharama kubwa ambayo isingeweza kufikiwa iwapo stika hizi zingeuzwa kwa fedha ya Tanzania.
“Kwa mujibu wa kiongozi wetu sidhani kama haya ndiyo yalikuwa makubaliano yetu. Stika moja tunanunua kwa shilingi 14, lakini unalipa kwa pauni na si shilingi ya Tanzania, hata hivyo tunauziwa kuanzia stika 100 na si chini ya hapo.”
Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alisema, “Kubwa zaidi tunalolalamikia sisi kama wasambazaji na wasanii ni kuuziwa stika hizi kwa fedha isiyo yetu, kwa nini iwe hivi, pauni kila siku inabadilika mara inapanda mara inashuka.”
Novemba alisema, “Wasanii wa muziki wanalalamika kuhusu hilo hasa wa muziki wa Injili. Wasanii wa muziki wa kizazi kipya wameamua kukacha kabisa albamu kutokana na ukweli kwamba hawauzi, lakini hata waliofurahia urasimishaji bado utata unakuja kwenye stika yaani hakuna afadhali tulidhani tutapata haki, lakini sasa mambo ndivyo sivyo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Five Effect, kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa kazi za wasanii, William Mtitu naye alisema, “Kuna uhaba wa stika hata hivyo tunanunua kwa pauni, wasanii tuliamua kusambaza kazi zetu wenyewe kutokana na tatizo la kutoendelea na Mhindi anatunyanyasa siyo siri akinunua kazi yako humdai tena anaitumia atakavyo.