Skip to main content

Hamahama ya wanasiasa yatikisa vyama

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja akizungumza na waandishi wa habari wakati yeye na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita (wa pili kulia), wakitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema.  Kulia ni Sheikh Sadick Burhani kutoka Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na Shura ya Maimam. Picha na Said Khamis 
By Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Wimbi la wanasiasa kuhama vyama wakati wa uchaguzi limekuwa la kawaida, lakini miaka 20 baada ya siasa za vyama vingi kurejeshwa, hali hiyo inaonekana kutikisa vyama hasa baada ya kutawaliwa na mawaziri, wabunge na madiwani.
Tangu Rais Jakaya Kikwete atoe hotuba yake ya mwisho kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, wanasiasa wamekuwa wakitangaza kukimbia vyama vyao, na hali hiyo ilikolezwa baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuihama CCM na kujiunga na Chadema mwishoni mwa Julai, baada ya jina lake kuenguliwa kwenye mbio za urais za CCM.
Sababu kuu ambazo zimekuwa zikitolewa wakati wanasiasa hao wanapohama ni majina yao kukatwa isivyo halali kwenye harakati za uchaguzi, kutofautiana kifikra na viongozi na kutotendewa haki.
Hadi jana, kwa mujibu wa uchambuzi wa gazeti hili, Chadema ndiyo inayoonekana kunufaika na safari za makada wanaotoka chama kimoja kwenda kingine, mtaji wake mkubwa ukiwa ni Lowassa, ambaye pia ni mbunge wa Monduli.
ACT-Wazalendo, chama kilichoanzishwa katikati ya mwaka jana na ambacho kinaongozwa na naibu katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Zitto Kabwe, ndicho kinafuatia kwa kunufaika na kuhama huko kwa makada, huku CCM ikishika nafasi ya tatu.
Kwa taarifa ambazo Mwananchi imezikusanya, zaidi ya madiwani 50 wamehama vyama vyao na kujiunga na vingine, kati yao 46 wakiwa wametoka CCM na UDP na kujiunga na Chadema na wanne wakitokea Chadema na kutua ACT.
Chadema pia imepata wanachama wapya sita waliokuwa wabunge wa  CCM, huku ikipoteza wabunge watano waliojiunga na CCM, Tadea na ACT ambayo imevuna wabunge wawili wa viti maalum kutoka CUF.
Wenyeviti watatu wa mikoa ya Singida, Shinyanga na Arusha, na mwenyekiti wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam, wameihama CCM na kujiunga Chadema. Katika orodha hiyo pia wapo wagombea ubunge waliotoswa katika kura za maoni na makatibu wa wilaya na mkoa wa chama hicho tawala.
Wachambuzi walonga
Wakati wanasiasa hao wakisema uamuzi wao unatokana na kutoridhishwa na mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, wa kura za maoni za ubunge na udiwani, kutofautiana kifikra na viongozi na vyama kukiuka misingi ya kuanzishwa kwake, wachambuzi wa siasa waliohojiwa na Mwananchi walikuwa na maoni tofauti.
“Tupo kwenye mfumo wa vyama vingi. Sasa watu wanaona vyama vyenye uwezo wa kuongoza nchi ni vingi na si kimoja tu,” alisema makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Dk Charles Kitima ambaye aliilezea hali hiyo kuwa ni kukua kwa demokrasia.
“Kwa kulitambua hilo, wanaona uwepo wa vyama vingi ni uhalisia wa utaratibu wa kisiasa na si maigizo tena. Kuhama chama kimoja kwenda kingine kunaonyesha kuwa kuna ukomavu wa kidemokrasia nchini. Ni jambo la kushukuru kama watu watahama kwa nia ya kuwawakilisha wananchi na kuwaletea maendeleo wanayoyatarajia.”
Hata hivyo, alisema mwanasiasa kuhama chama kimoja baada ya kushindwa katika kura ya maoni ni jambo ambalo wananchi wanapaswa kujiuliza kwanza.
“Tujiulize huyu mtu anahama baada ya haki zake kubanwa huko alikotoka au anaenda upande wa pili akaongeze nguvu. Tujiulize maswali hayo,” alisema.
Alisema wananchi ni lazima wajue nia na malengo ya wanachama kuhama na kuvitaka vyama vya siasa kuheshimu haki za msingi za binadamu.
Wakati Dk Kitima akitaka kuwapo kwa umakini na wanasiasa wanaohamia vyama, mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Emmanuel Mallya anawatetea akisema kuhamia chama kingine si uchu wa madaraka.
“Kila mtu ana uhuru wa kufanya uamuzi kuchagua chama anachokitaka,” alisema Mallya.
“Kama anaondoka chama fulani kwenda kingine, wananchi wanapaswa kumhoji nini anataka kuwafanyia na sababu za kuhama kwake. Mfano mimi nikihama chama fulani na kwenda kingine na nikachaguliwa kuwa mbunge maana yake watu wananipenda, huwezi kusema nina uchu wa madaraka.”
Lakini mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema suala la wanasiasa kuhama vyama ni dalili kuwa kuna tatizo kubwa la kidemokrasia.
“Hili suala halina majibu mepesi. Ni jambo linalohitaji uchambuzi mkubwa. Kwa kifupi niseme kwamba hiyo ni dalili ya tatizo kubwa la kidemokrasia,” alisema Bashiru.
“Yanayoendelea ni dalili kwamba kuna ugonjwa katika siasa na uchumi wetu unakua. Tuhangaike na chimbuko la ugonjwa huo kuliko kutafuta kupoza hizi homa na dalili zinazojitokeza.
“Tabibu mzuri ni yule anayetafuta chimbuko la ugonjwa badala ya kuhangaika na dalili ingawa dalili zinaweza kumuongoza katika kufuatilia ugonjwa.”
Alisema wanasiasa kuhama vyama ni ugonjwa uliokomaa na unaonekana kuwa sugu kwa siasa na uchumi nchini.
“Tunayoyashuhudia na mengine tunayoyaona mazuri au tunayoyanung’unikia na kuyaona mabaya huku watu wakiwa na hofu na matumaini, vyote ni viashiria kwamba hali ya kiafya ya mfumo wetu wa kisiasa na kiuchumi si nzuri. Unahitaji utulivu kutafuta chanzo,” alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema wengi wamehama kutokana na kushindwa kwenye kura za maoni, huku akirudia kauli yake kuwa makada hao “walikuwa oili chafu” na chama hicho kitasonga mbele na mafuta safi.
Naye mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, alisema kwenye mtandao wa kijamii mwishoni mwa mwezi uliopita kuwa waliohama chama hicho (Chadema) walikuwa hawaonekani kikazi.
“Ukiangalia wote waliohama, utaona walikuwa anonymous,” alisema Lissu.
Baada ya Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za urais ndani ya CCM Julai 11 na siku iliyofuata Mkutano Mkuu kumpitisha Dk John Magufuli kuwania urais, ilionekana kama chama hicho tawala kimeshadhibiti hamaki iliyotokana na mchakato huo na kuwa kitu kimoja kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Hali ilianza kubadilika baada ya kuibuka taarifa kuwa mbunge huyo wa Monduli alikuwa kwenye mazungumzo na Ukawa kuhusu uwezekano wa kupewa fursa ya kutimiza ndoto yake ya urais kwa kupitia vyama vya upinzani.
Uamuzi wake wa kujiunga Chadema Julai 28 ulibadili upepo wa kisiasa, kuanzia kwenye mbio za urais, licha ya wabunge wawili wa CCM, James Lembeli na Ester Bulaya kutangulia kutangaza kujiunga na Chadema.
Akitangaza uamuzi wake wa kujiunga Chadema, Lowassa alimkariri Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje.
Alisema amekua na kulelewa na chama hicho kikongwe, lakini CCM imeondoka kwenye misingi yake ya wali.
Takribani mwezi mmoja sasa kumekuwa na wimbi kubwa la madiwani wa CCM na UDP kuhamia Chadema, wakati huohuo wabunge wa chama hicho kikuu cha upinzani kutangaza kuhamia CCM, Tadea na ACT- Wazalendo.
ACT kinachoongozwa na Zitto Kabwe pia kimepata wabunge wapya kutoka Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Wabunge, madiwani waliohamia     Chadema
Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli, anaongoza orodha ya wabunge waliohama vyama vyao, ambayo pia inamjumuisha Bulaya, Lembeli, Said Nkumba, Goodluck Ole Medeye na Dk Makongoro Mahanga. Wote walieleza
kutopendezwa na mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM pamoja na kutotendewa haki.
Aliyeanguka kwenye kura za maoni za ubunge ndani ya CCM wilayani Kilindi, Magawa Ndaro na madiwani watano wa chama hicho nao walihamia  Chadema wakidai kutotendewa haki.
Madiwani hao na kata zao katika mabano ni Evans Mushi (Msanja), Marco Mobeshi (Kilindi Asilia),Gasper Kayaya (Rwande), Wilfred Lukmayi (Masagalu) na Mohammed Makengwa (Songe).
Wengine waliojiunga na Chadema na kueleza sababu hiyo ni diwani wa Kata ya Kahororo na mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Manispaa ya Bukoba, Chifu Marumuna.
Madiwani wengine 18 wa CCM Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro walitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema, sambamba na wengine 10 wa UDP na CCM wilayani Bariadi.
Waliohamia ACT
Chadema si chama pekee cha upinzani kilichonufaika na wimbi hilo la kuhamahama, bali chama kipya cha ACT Maendeleo, ambacho kinaonekana kufanya kazi kubwa ya kujitangaza.
Aliyekuwa mbunge wa Kasulu Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Moses Machali alihamia ACT na kupitishwa kugombea tena ubunge wa jimbo hilo. Katika maelezo yake Machali alisema amehama NCCR kutokana na kutoelewana na viongozi wake wakuu.
Wabunge wanne wa viti maalumu walihama Chadema, watatu kati yao kutangaza kuhamia ACT na mmoja CCM. Wabunge hao ni Chiku Abwao, ambaye amepewa fursa ya kugombea Jimbo la Iringa Mjini, Mhonga Ruhwanya na Ana-MaryStella Mallac huku Leticia Nyerere akirejea CCM.
Waliojiunga na chama hicho wakitokea CUF ni Amina Amour na  Mkiwa Kimwanga (wote viti maalum).
Kwa upande wa udiwani, Azuri Mwambagi, aliyekuwa diwani kwa tiketi ya Chadema, amejiunga na ACT sambamba na madiwani wanne wa Chadema waliomaliza muda wao katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Madiwani hao ni aliyekuwa naibu meya wa manispaa hiyo na diwani wa Kibirizi, Rashidi Ruhomvya, Adam Shabani (Rubuga), Hawa Saidi na Tatu Rajabu (Viti Maalum).
Katika orodha hiyo yupo aliyekuwa mgombea ubunge wa Chadema jimbo la Kalenga, Mwanahamisi Muyinga ambaye aliangushwa katika kura za maoni.
Waliohamia Tadea
Chama kingine kilichonufaika na wimbi hilo ni Tadea ambayo ilimpata aliyekuwa mbunge wa Chadema jimbo la Maswa Magharibi, John Shibuda.
Waliohamia CCM
CCM, ambayo imemaliza mchakato wake wiki hii, nayo ilivuna Aliyekuwa mbunge wa Chadema wa Jimbo la Mpanda, Said Arfi, ambaye aliangushwa katika kura za maoni za chama hicho kikuu cha upinzani.
Wenyeviti
Orodha ya wanasiasa waliohama pia inajumuisha wenyeviti wa mikoa baada ya makada watatu wa CCM- Mgana Msindai (Singida), Onesmo Ole Nangole (Arusha) na Hamisi Mgeja (Shinyanga) kuhamia Chadema, sambamba na mwenyekiti wa zamani wa chama hicho mkoani Dar es Saalam, John Guninita.
Katika maelezo yao, Guninita na Mgeja walisema uamuzi wao unatokana na CCM kupoteza mwelekeo, kuendeshwa kwa ubabe bila kujali demokrasia, hasa katika mchakato wa kumpata mgombea wake wa urais.
Ole Nangole alihamia Chadema pamoja na katibu wa Uenezi na itikadi wa CCM mkoani Arusha, Isack Joseph huku wote kwa pamoja wakieleza wazi  kuwa wanamfuata Lowassa.
Pia mwenyekiti wa zamani wa UVCCM mkoani Mbeya, Reginald Msomba pamoja na George Mwakalinga aliyeshindwa kura za maoni kusaka ubunge Jimbo la Kyela kupitia chama hicho, walitangaza kujiunga Chadema pamoja na katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Longido, Tostau Mollel.

Popular posts from this blog

MAJINA YA WASHIRIKI NA WA WEZESHAJI WA FILM YA HOUSE GIRL!

CAST SELEMANI MOHAMED / BUNTO ANDREW / C-O YORAM MWETA / MGANGA MWANTUMU / MKE WA C-O JOHN / MCHUNGAJI BI FURURATU / JINI WAOMBOLEZAJI SAUMU HUSENI HASHIMU BABA RASTA MAN YOHANNA TAMILWAI SAIDI MWALUBADU SEMY STIR SELEMANI MOHAMEDI  AND ANDREW C-O LOCATION ATHUMANI HAMADI MAKE UP MWASHAMBA RAMADHANI BEDUI DEREVA DAUDI SPOONSER SAIDI SHABANI AND THE FRESH2012 GLOB SOUND PRODUCER J-B LIGHT YOHANNA TAMILWAI THENK YOU THE FRESH ENERTAINMENT AND THE FRESH2012 BLOG CONTACTS 0653785027 +255714091786 ZAIDI TEMBELEA www.the-fresh.blogspot.com ADRESS Thefresh@ymail.com AU Saidshabani60@gmai.com

Sababu ya Alicia Keys kumuita mwanae Misri (Egypt)

Siku chache kabla ya Mother’s Day Alicia Keys alihojiwa kwenye talk show iitwayo  ‘The Conversation’ inayotayarishwa na Demi Moore na mtangazaji akiwa Amanda de Cadenet. Waliongea mengi kuhusu maisha yake kama mama, umbo lake baada ya kuzaa, kunyonyesha na sababu iliyomfanya amuite mwanae Misri. “Well, Misri ilikuwa safari muhimu katika maisha yangu” Alisema Alicia. Ilikuja katika pointi ambayo nilikuwa nimefanya kazi mno bila kupumzika na sikuwa na idea yoyote kuhusu kuchukua likizo ya kweli na ilikuja katika muda huo ambao niliihitaji.  Hivyo nilipoenda, ilinipa nguvu sana, ikanifungua macho, safari ya kihistoria, yenye nguvu na experience ya pekee iliyonifanya niipende Misri.  Alicia, Demi na Amanda Hivyo  ulipokuja wakati wa kumpa jina mtoto wetu, nililipenda, wote tulilipenda na tuliamua miezi kadhaa hata kabla hajazaliwa” Egypt na baba yake Swizz Beatz Kuhusu kwanini alienda peke yake nchini Misri alisema “Muda huo nilihitaji sana kwenda

Tuhuma nzito : Magufuli, Mwakyembe, Lukuvi kufikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge

Dk John Magufuli   Dar es Salaam.   Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema itawafikisha kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akiwatuhumu kwa kulidanganya Bunge. Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe baada ya kumhoji Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert Mrango kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka wa fedha 2011/2012. Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya mwaka huo kiasi cha Sh348,075,000,000 fedha za ndani zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililotajwa kuwa ni la mradi maalumu (Special Road Construction Project) hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa bungeni. “Ni vizuri leo uiambie kamati fedha hizi ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa jambo gani. Tunajua kwamba