Ukiwa msikilizaji mzuri wa muziki, hasa wa kizazi kipya kuna wakati utakubaliana na kauli isemayo katika nyimbo bora zilizotoka mwaka huu ambazo zina mafunzo ambayo mabinti hupenda kuyasikia, hutaacha wimbo uitwao “Subira” wa kijana mdogo kutoka Tanga, Kassim Hemed Mganga.
Ukimuona kwa mbali unaweza ukahisi kuwa ni kiumbe mzito, lakini ukimpa muda wa kurembesha jukwaa lako kwa burudani, utagundua kuwa umbo lake na sanaa anayofanya ni vitu viwili tofauti.
Ana uwezo wa kusherehesha kwa takriban masaa matano bila kuchosha mashabiki wake.
Kibao chake cha “Subira” ndiyo habari ya mjini; kwenye pub, baa, klabu, bodaboda, bajaj, redioni na simu za mikononi ni “Subira, Subira Subira”.
Ni kibao kilicho katika miondoko ya pwani, hasa chakacha, na chenye mashairi yanaotahadharisha, kufundisha na sauti ya kuburudisha ambayo inanogeshwa na Christian Bella ambaye amempa shavu Kassim kwenye wimbo huo.
Kassim Mganga ni mmoja kati ya vijana walioingiza ladha tofauti kwenye muziki wa bongo fleva.
Ni msanii mwenye nidhamu anapokuwa katika maisha ya kawaida na ambaye hawaamini kabisa kwamba ili kuwa staa, ni lazima utengeneza kashfa itakayofanya jina lake liwe midomoni mwa watu kwa angalau siku mbili tatu.
Ndiye yule msanii aliyeimba, “Nakuimbia”, kisha “Awena” halaf akaimba “Haiwezekani”, “Tajiri wa Mahaba”, “Amore na I Love You”. Zote hizo huzitoa kwa nyakati tofauti, halafu hutulia kabla ya kutoa nyingine kwa wakati muafaka kiasi cha kufurahiwa na mashabiki wake.
Msanii huyo anayetoka katika familia ya wanamuziki anaamini katika muziki mzuri.
“Kinachonisaidia mpaka leo ni muziki mzuri kwa mashabiki na si kitu kingine chochote,” Kassim Mganga anaiambia Starehe.
Bila shaka, muziki wake usingekuwa hiyo, angekuwa ameshapotea kutokana na hali halisi ya soko la muziki Tanzania.
Alikoanzia
Kassim Mganga hajui kama muziki kwake ni kipaji ama urithi, lakini anakiri kwamba muziki ameukuta ukumbini.
Alizaliwa katika familia ambayo alikuta baba ni mwanamuziki, na mama anaimba. Akakulia katika familia ya muziki na hivyo akaaanza taratibu kuwa mwanamuziki.
Baba yake, Hemed Salim Mganga alikuwa bendi la Legho Stars, na mama aliimbia vikundi vya Bandari Modern Taarab ya mkoani Tanga na Coast Modern Taarab.
“Unajua kwenye tungo za wazee wetu, lazima ukiandika kitu kiwe na mafunzo na kuburudisha na ndio nimekulia katika mazingira hayo,” anasema Kassim Mganga.
“Na ndio maana naamini katika maadili zaidi kuliko kufanya hili au lile ili nisikike. Watu watausikia muziki wangu na watanitambua kupitia huo.”
Kassim alianza kuimba pamoja na baba yake kwenye bendi ya Legho Stars.
“Nilikuwa naongozana na baba kwenda densini na kwa kuwa wakati ule dansi lilikuwa likianza mchana, nilianza kushiriki kuimba,” anasimulia.
“Wimbo pekee niliokuwa nikiimba ulikuwa “Ngalula”. Ilikuwa lazima nipande na baba niuimbe hasa wakati wa sikukuu ambazo kulikuwa na dansi la watoto.”
Kinachompa uhai kimuziki
Anasema hivi sasa muziki ambayo ukipigwa, huulizi mara mbili, unamjua kabisa huyu ni Kassim Mganga, ambaye kwa sasa anaitwa Gwiji.
Anasema mpango wake ni kuuweka mbele utamaduni wa pwani ambao kwa kiasi kikubwa burudani yake imetawaliwa na tungo mwanana za kimahaba.
Na ndio maana, kwanza haachi kutaja anakotoka katika mwanzoni mwa kila tungo, na pia ule utajiri simulizi za mahaba za pwani ndio unanogesha mashairi yake, huku akibaki kuwa ‘jeshi la mtu mmoja’.
“Sina meneja, na nina uhakika ningekuwa naye, muziki wangu ungekuwa mbali sana. Najisimamia na ndio siri ya kufika nilipo,” anasema Kassim ambaye aliwahi kuwa na kundi la Tip Top Connection.
Lakini anasema kujisimamia ni kazi ngumu.
“Kuna kazi inabidi uachie watu wafanye ili wewe uendelee na kazi ya kutengeneza muziki mzuri tu. Lakini sasa ukiangalia Tanzania, mameneja ni wachache, wengi hufanya kazi ya udalali wa wasanii na sio umeneja,” anasema.
Maonesho yake
Unaweza usimuone katika matamasha, lakini Kassim ana miaka 13 katika muziki ambao ndio pekee unapeleka mkono kinywani. Anakula, anavaa, anasomesha watoto watatu, na anaendesha gari zuri la kawaida kwa kutumia muziki.
Ila sasa ukimuuliza muziki wake anapiga saa ngapi? Maana mara nyingi haonekani kwenye matamasha, jibu lake ni kwamba anatumbuiza kwenye sherehe za harusi.