Mbeya. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa jana alipokewa na maelfu ya watu mjini hapa ambao kwenye uwanja wa Ruanda, Nzovwe, aliwaambia wananchi kuwa hatataka mchezo katika serikali atakayoiongoza.
Pamoja na Jeshi la Polisi kutangaza kuzuia msafara wakati wa ziara ya waziri huyo mkuu wa zamani, hali ilikuwa tofauti jana wakati zaidi ya magari 20 yalimsindikiza kutoka Uwanja wa Ndege wa Songwe huku wananchi wakijitokeza barabarani kumshangilia hadi kwenye uwanja huo, ulio nje kidogo ya mji wa Mbeya ambako alihutubia.
Polisi walinda msafara
Msafara wa Lowassa uliwasili mjini hapa kwa kutumia ndege mbili, ya kwanza ikiwa imebeba waandishi wa habari wapatao 10 na nyingine iliyombeba mbunge huyo wa Monduli ambayo iliwasili saa 8:20.
Umati wa watu ulikuwa ukimsubiri nje ya uwanja huo na alipotoka ilianza safari ya kuelekea katikati ya jiji na msafara wa zaidi ya magari 20 pamoja na pikipiki.
Polisi walitanda barabarani, huku vijana wa Red Brigedi waliovalia sare nyeusi na miwani wakiwa wamesambazwa barabara yote.
Maeneo ambayo msafara ulipita kwa shida kutokana na umati wa watu kufurika ni Mbalizi, Mafiati Mwanjelwa, lakini polisi walifanya kazi ya ziada kuwaondoa watu waliokuwa wakitaka kuandamana kuusindika msafara huo.
Lowassa aliambatana na mgombea mwenza, Juma Haji Duni, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na kulakiwa na viongozi wa mkoa pamoja na mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Sugu.
Akizungumza baada ya kukaribishwa kuhutubia na Duni Haji, Lowassa alianza kwa kibwagizo cha “mchakamchaka chinja” na kabla ya kuwashukuru wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kufurika hadi pomoni kwenye uwanja huo.
“Sitaki mchezo,” alisema Lowassa ambaye amekuwa akizungumzia uendeshaji wa Serikali kwa mtindo wa mchaka mchaka.
“Nataka maendeleo. Nataka Jiji la Mbeya liwe la kimataifa wakati wa Serikali yangu na litakuwa kama nchi ya Swaziland,’’ alisema akilifananisha jiji hilo na nchi hiyo ndogo iliyozungukwa pande zote na Afrika Kusini.
“Nitahakikisha Uwanja wa Ndege wa Songwe unakuwa wa kimataifa.”
Lowassa, ambaye alipata zaidi ya watu 50,000 mjini hapa wakati alipokuwa akisaka wadhamini wa urais kwa tiketi ya CCM, alisema Serikali yake pia itawajali walimu na wakulima, huku akisisitiza kwamba watakaochelewesha pembejeo watakiona cha moto.
Akizungumza polepole, Lowassa alisema katika Serikali yake hatataka mchezo katika kazi na kwamba mawaziri wake watachapa kazi saa 24 kuwahudumia wananchi.
Kuhusu kiu ya wananchi waliotaka kujua kauli yake kwa polisi, alisema polisi wanatenda kazi huku wakitaka mabadiliko ya kupata mshahara mnono na kwamba ataboresha mahitaji ya wafanyakazi kwa ujumla.
Awali akiwakaribisha wageni, Sugu aliwashukuru wakazi wa Mbeya kwa kile alichokieleza kuwa ni kuleta mizuka kwenye uwanja huo kutokana na kufurika watu wengi. “Karibu Mbeya wageni, hapa siyo mafuriko ni gharika... kilichobaki ni kupiga kura ya kukuchagua wewe Rais Lowassa,’’ alisema.
Sugu alisema goli la mkono la CCM litazuiwa na beki makini Lowassa na kutoa onyo kwamba CCM wasidiriki kutumia kadi bandia za wapiga kura.
Naye Mbatia alisisitiza suala la Watanzania kulinda amani na upendo na kuwasihi wakazi wa Mbeya wasikubali kufanya vurugu katika kipindi chote cha kampeni na uchaguzi.
Wabunge wawili wajiunga Chadema.
Wakati Lowassa akipata wadhamini, Chadema ilipata neema tena wakati wabunge wawili wa CCM, Dickson Kilufi wa Mbarali na Luckson Mwanjale wa Mbeya Vijijini walipotangazwa kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani.
Hata hivyo, Mbowe alimkabidhi kadi Kilufi pekee baada ya Mwanjale kutofika eneo hilo licha ya kuonekana uwanja wa ndege.