Tume ya Uchaguzi (NEC) imewaengua wagombea urais wa vyama vya Ada/Tadea, DP, CCK na AFP leo kwa maelezo kuwa wamekosa vigezo vya kugombea nafasi hiyo kubwa ya uongozi hapa nchini.
Kwa mantiki hiyo, Mchungaji Christopher Mtikila (DP), Godfrey Malissa (CCK) na John Chipaka (Ada-Tadea) hawatashiriki katika kinyang’anyiro hicho baada ya fomu zao kuonekana kuwa zina kasoro huku mgombea urais wa AFP, Omari Sombi akiungana na wanasiasa hao kutogombea baada ya kushindwa kurejesha fomu ya urais.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, wagombea wa vyama vinane kati ya 12 vilivyochukua fomu, wamekidhi matakwa ya sheria ya mchakato huo, hivyo wanaruhusiwa kuanza kampeni rasmi kesho.
Amewataja wagombea waliopitishwa na NEC ni Dk. John Magufuli (CCM), Edward Lowassa (Chadema), Fahmi Dovutwa (UPDP), Macmillan Lyimo (TLP) na Chief Lutalosa Yemba (ADC).
Wengine ni Anna Mghwira (ACT-Wazalendo) na Hashimu Rungwe (Chaumma) na Malik Kasambala (NRA).
(C) Mwananchi
Je, Tutarajie Mchungaji Christopher Mtikila Kutinga Mahakamani kupinga katazo hilo??