Dar es Salaam. Uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitisha kambi ya timu ya Taifa wakati klabu zikiwa kwenye maandalizi ya msimu mpya wa ligi, umepokewa kwa hisia tofauti na wadau wa mchezo huo, baadhi wakizilaumu Yanga na Azam kwa kuzuia wachezaji wao na wengine wakiliponda shirikisho hilo kwa kutokuwa makini.
Kocha Charles Mkwassa amelazimika kuita wachezaji 10 wa ziada kujaza nafasi za wachezaji kutoka Yanga na Azam zilizoweka kambi nje ya Dar es Salaam. Stars inajiandaa kwa mechi ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Nigeria.
Wakizungumza na gazeti hili, wadau hao walisema Yanga na Azam hazijafanya kitu kizuri, lakini pia wakaeleza kuwa TFF ilitakiwa kupanga ratiba za klabu kwa kuangalia tarehe za mechi za Stars.
Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema Yanga na Azam hazikupaswa kuwazuia wachezaji wao kujiunga na kambi ya Stars kwani mechi ya Ngao ya Jamii ni ya kawaida, ukilinganisha na ile dhidi ya Nigeria.
“Tumeshuhudia Ulaya ambako ndiko wenye mpira wao inapofika timu ya taifa ni suala jingine, hivyo sioni kama ni sahihi kwa Yanga na Azam kuwazuia wachezaji wao kujiunga na kambi,” alisema Bwire.
“Inapofika hali ya kugongana kwa ratiba kama hivi unaangalia umuhimu wa mechi. Wangewaachia walioitwa Stars wajiunge na kambi, hao waliobaki wangecheza hiyo mechi ya Ngao ya Jamii,” alisema Bwire.
“Ndiyo maana timu ikasajili wachezaji 30 ili kama wengine hawapo, wengine wanachukua nafasi, lakini kwa jinsi hali hii ilivyojitokeza inaonyesha kabisa Yanga na Azam ni waoga. Wanawategemea wachezaji fulani na bila wao wanaona hakuna timu jambo ambalo siyo sahihi.
“TFF wanatakiwa kubadilika, wanapopanga ratiba ya ligi waaangalie na kujiridhisha kuwa haiingiliani na mashindano mengine hasa yanayohusu timu ya Taifa.”
Meneja wa Mwadui, Khalid Adam alisema Azam na Yanga ziko sahihi kuwazuia nyota wao kujiunga na Taifa Stars kwani hata klabu nyingine duniani zinafanya hivyo kwa masilahi ya klabu hizo.
“Kama tunafuata mfumo wa dunia ,timu ya Taifa inafanya maandalizi siku nne hadi tano kulingana na kalenda ya Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa, kuwazuia wachezaji si kwa klabu za hapa nchini kwani kuna wakati hata Barcelona iliwahi kumzuia Lionel Messi kujiunga na timu ya Argentina, inategemea hayo mashindano ya nini na je ni muda wa kalenda ya Fifa.