Serikali imependekeza marekebisho ya sheria ya kudhibiti dawa za kulevya itakayotoa hukumu ya kifungo cha maisha na kufuta kipengele kwenye sheria ya sasa kinachompa mshtakiwa nafasi ya kulipa faini. Sheria iliyopo sasa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya ya mwaka 1995 (Sura ya 95, Ibara ya 16) inasema, endapo mtu atakamatwa kwa kosa la kumiliki, kusafirisha, kuzalisha au kutengeneza mashine ya dawa za kulevya, atahukumiwa kifungo cha maisha jela au kulipa faini ya Sh10 milioni. Hatua hiyo inakuja wakati idadi ya Watanzania wanaosafirisha, kuzalisha na kutumia dawa hizo ikiongezeka hapa nchini. Pamoja na mapendekezo hayo, wadau mbalimbali wamesema kufanyika kwa maboresho hayo hakutasaidia kupambana na tatizo lililopo hivi sasa, ikiwa maadili ya wananchi na viongozi yaliyoporomoka hayatarekebishwa. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema sheria yoyote itakayowekwa haiwezi kuwa ‘mwarobaini’ wa kutibu tatizo la dawa za kulevya hapa nchini ka