RAIS Jakaya Kikwete amekiri kuwapo mazingira mabovu ya Jeshi la Magereza nchini na kulitaka jeshi hilo kubuni njia za uzalishaji wa bidhaa zao zitakazoweza kuwaletea faida na taifa kwa ujumla.
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana kwenye sherehe za kumaliza kozi kwa maofisa 104 wa ngazi ya juu wa Jeshi la Magereza yaliyofanyika katika Chuo cha Taaluma na Urekebishaji Ukonga.
Alisema mazingira mabovu yanachangiwa na wingi, msongamano wa wafungwa na watuhumiwa katika magereza hali inayofanya jamii kuwa na malalamiko ya mara kwa mara.
“Kila mwaka wanaotetea haki za binadamu wanapopita kwenye magereza zetu, tunakuwa tunashindwa kwenye suala la msongamano ndani ya gereza na hii inaonyesha magereza tulizonazo 126 hazitoshelezi kulingana na kasi ya ongezeko la uhalifu.
“Hii inajidhihirisha wazi kwani kila inapofika sikukuu za Muungano Aprili 26, tunasamehe wafungwa, lakini ikifika Desemba 9 Sikukuu ya Uhuru unakuta wameongezeka mara mbili,” alisema Rais Kikwete.
Alisema ili jeshi liweze kutimiza majukumu yake vizuri, ni lazima kuwe na watu, ujuzi na vitendea kazi ambavyo bado vimeonekana kuwa ni changamoto kwa jeshi hilo.
Pamoja na hali hiyo alilitaka Jeshi la Magereza kuwa na malengo ya kuboresha viwango bora.
“Jeshi linasifika kwa kuzalisha chakula na bidhaa bora, lakini kwenye uzalishaji wenu msiishie kweye mazao ya chakula, bali muangalie na mazao ya thamani pamoja na kuanzisha viwanda vikubwa na kilimo cha umwagiliaji,” alisema Rais Kikwete.
Aidha alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linaharakisha mchakato wa Sera ya Taifa ya Magereza na mpango kazi wake ambao ameutaka uwasilishwe kabla hajaondoka madarakani Oktoba mwaka huu.
Awali Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Minja, alisema jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo la ongezeko la mahabusu, upungufu wa fedha kutokana na gharama kubwa ya uendeshaji, makazi ya maofisa na askari, ofisi chakavu na suala la usafirishaji.
“Mazingira yetu hayaridhishi sana, nyumba ni chache na zilizopo ni chakavu, pia magari kwa ajili ya usafirishaji bado ni tatizo sambamba na majengo machache ya mahakama,” alisema Kamishna Minja.